RSS

Tag Archives: Vitali

Chanjo

Mwanzo wa Chanjo

Mwanzo wa Chanjo

Mara nyingi imezungumzwa na kujengeka katika jamii yetu ya watanzania, pia hata jaamaa zetu nchi za jirani kuwa Rushwa ni jambo ambalo halitaisha, wengine wanathubutu kusema kuwa dunia hii bila rushwa si dunia.

Rushwa imewafaa wabinafsi wengi, imewanufaisha na kuwadhalilisha watu wengi katika jamii mbalimbali Duniani, imefanywa kuwa ni kitu cha muhimu kabisa katika maisha yetu.

Tunaisema vibaya na kuiandika vibaya rushwa kutokana na ubaya wake, wakati mwingine tunafanya hivyo ilitupate kibali kwa watu au kuungwa mkono na wanyonge au waathirika wa rushwa, lakini kusema ukweli ndani yetu bado hatujakubali ukweli ambao wote tunaujua kuwa rushwa ni tatizo.

Tangu kiongozi mkubwa wa kisiasa mpaka mtu wa kawaida kabisa katika jamii anaamini kuwa rushwa haitaisha, watu wanaishiriki rushwa kwa sababu fulani, wakati mwingine kwa kuamua na wakati mwingine kwa kulazimika. Ninaamini kuwa rushwa ina mwisho, nitaendelea kuamini hivyo kwa kuwa huo ndio ukweli wenyewe.

Ingawa nyimbo za kuwaweka huru watanzania kutoka katika makucha ya rushwa zinaonekana ni hotuba ya mwendawazimu tu.

Rushwa imesimama imara kwa kujiamini, mawakala wake wamekuwa na nguvu kupindukia. Wasanii na wana habari ndio tumaini pekee la ukombozi wa mtu wa kawaida dhidi ya rushwa, lakini baadhi yao ndio wamekuwa mawakala wa rushwa, hatupendi kusema maneno haya lakini inapobidi inabidi tuseme ingawa tunajuwa tutaumizwa kwa kusema haya. Wazazi wamekata tamaa, walezi wa kiimani na kimaadili wanasema “rushwa haiepukiki na hivyo ndivyo ilivyo tutafanyaje?”

Naishi katika mazingira ambayo watu wanalia kila siku, wanalalamika kilasiku kuhusu rushwa, watu ambao wanashindwa kumudu matibabu, watu ambaowanashindwa kupata huduma ya elimu ipasavyo, watu wanaopoteza maisha yao na jamaa zao kutokana na upevu wa rushwa. Siitazami tena rushwa kwa macho ya kawaida, naitazama kwa roho na naichunguza tabia yake ninagundua kitu.

Nikawatazama watanzania, nikawatazama waafrika, nikaitazama dunia sioni tena umuhimu wa nyimbo za kuwaburudisha na kuwapumbaza watanzania, kwa hali iliyopo siwezi kusema wasanii wote tubadilike bali wanaoweza kusema na njaa zao wafanye hivyo na tuangalie ni namna gani tunaikoa nchi yetu na sio ni namna gani tunajinufaisha kifedha.

Siogopi tena kusema kwamba naifahamu rushwa vilivyo, nayajua madhara yaliyoletwa na rushwa, nayajua maafa yatakayoletwa na rushwa, nawajua mawakala wa rushwa, zaidi na zaidi naujua umri wa rushwa, nathubutu kukwambia ukweli huu, kitu bora na cha ajabu ni kwamba kifo na uhai wa rushwa vipo katika ulimi wangu, vipo katika akili na roho yako.

Bado kidoogo sana tutamjua nani ni mwanamapinduzi wa kweli.

Huu si wakati wa nadharia, kama tunaitakia mema jamii yetu, Siafu waliamua kujenga daraja kwa miili yao, kwa kushikana na kufungana wenzao waliweza kwenda upande wa pili kwa kupita juu yao…. Wanajulikana kwa matendo yao kamwe si maneno yao.

Leo hii nakupa CHANJO dhidi ya rushwa na ubinafsi, nakupa uwezo wa kusema ‘rushwa kufa’ na rushwa ikafa.

Nimepita redioni na kugawa miziki ili uisikilize kwa makini, ipenye roho na akili yako kupitia masikio yako na iwe kinga yako dhidi ya rushwa. Wengi walifikiri kwamba hizi ni hadidhi tu, la haya ni maisha halisi.

Nimepita katika shule na mitaa ya Bagamoyo, nimekaa na watu na kuwapa chanjo kwa kuwapigia muziki, kukaa na kujadili nao juu ya janga hili.

Mnamo tarehe 03/02/2011 nilianza kazi hii bila kutumwa wala kushinikizwa na mtu wala shirika lolote. Majira ya saa tatu kamili kazi hii ilianzia katika shule ya msingi Mbaruku, kisha Mwanamakuka, kisha Majengo, kisha shule ya sekondari Dunda, na baadaye kumalizia na shule ya msingi Jitegemee. Watoto, wanafunzi wasio pungua 2000, walimu wasio pungua 9 walipata chanjo na kula kiapo cha kuikataa rushwa. Tarehe 04/02/2011 niliendelea katika shule ya msingi Pande, kisha shule ya msingi Mwambao, wanafuzi wasiopungua 500, walimu 7 walipata chanjo na kula kiapo.

Tarehe 05/02/2011 nilifanya onesho katika eneo la wazi Bagamoyo mjini kwenye viwanja vya Toptop, wakaazi wa bagamoyo wa umri tofauti tofauti wasio pungua 1000 walipata chanjo.

Tarehe 08/02/2011 nilikwenda shule ya sekondari ya Kiromo, wanafunzi 600 walimu na wafanyakazi wa shule 6 walipata chanjo na kula kiapo cha kuikataa rushwa. Jioni ya tarehe hiyo nilimaliza kwa kuwapa chanjo wanachuo TaSUBa na wakazi wa jirani na chuo hiki cha sanaa bagamoyo wasio pungua 400.

Safari hii iliaendelea mkoa wa Dar es salaamu, kisha tena Pwani, Morogoro, mpaka Dodoma. Panapo majaaliwa tutafika Singida, Tanga na Kilimanjaro.

Tarehe tulifika Dodoma kwa lengo la kufikisha Waraka wa Chanjo wenye kurasa tano unaowataka mawaziri na wawakilishi wafikirie namna ya kuboresha huduma katika jamii ambazo zinapelekea watanzania wengi kushiriki au kushirikishwa katika Rushwa. Pia likuwa ni kuwasilisha ujumbe kwa njia ya muziki, ujumbe ambao niliagizwa na watanzania wa kawaida. Mimi na wenzangu watatu tulifika Dodoma jumatano ya tarehe 16 februari, tarehe 17 asubuhi tulienda bungeni kuomba ruhusa kumuona Spika wa bunge ili kukabidhi waraka na kopi za albamu ya muziki ya Chanjo. Siku hiyo hatukufanikiwa kupata ruhusa, baada ya usumbufu mkubwa na vitisho getini kutoka kwa askari na wahusika wengine wa mlangoni jioni iliingia na siku ikaisha bila ruhusa. Hatukubali kuondoka mpaka tulipopata ruhusa ya kukutana na msaidizi wa Spika Bw. Berege, hatukuweza kumkabidhi barua zetu sitini na nne zinazotakiwa kuwafikia mawaziri wote, spika na katibu wa bunge kwa kuwa msimamo wetu ulikuwa ni kumfikishia Spika na kumkabidhi ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wahusika. Siku iliyofuata yaani tarehe 18 februari 2011, tulifika mapema asubuhi, mara hii tulipata ruhusa ya kuingia ktk ofisi ya spika, haikuwa rahisi kuonana naye lakini tuliridhika na ukweli, hivyo tulikutana na Katibu wa spika Bw. Eliufoo na kumkabidhi kwa maadishi.

Pamoja na hayo yote mpaka sasa sijapata matokeo ya ujumbe huo kwa walengwa wote yaani wawakilishi wa vyama na Mawaziri wote. Spika na katibu wa bunge pia wamekaa kimya.

Yawezekana wanafikiri kuwa huyu ni mpuuzi fulani anajaribu kujifurahisha au hawajaona umuhimu wa huu ujumbe kwao maana wengi wao kitu kizuri na chema kinasemwa na mtu fulani na sio Vitali Maembe, mtoto yatima fulani ambaye Baba yake alikuwa mtumishi mdogo tu wa Serikali ambaye baada ya kufa kwake hata mafao yake yameonekana kuwa hayastahili kwenda kwa mwanae sababu ya unyonge wa kielimu wa yatima huyu na ubabe wa kirushwa wa mifumo yao . Lakini wangejaribu kufikiri ni nani aliwahi kuandaa albamu ya muziki ili kuinusuru Tanzania na Afrika yake bila msaada? Au ni nani aliwahi kusafiri mtaa hadi mtaa. Kijiji hadi kijiji, Mji hadi mji akijaribu kuwaelimisha watanzania wenzake na kuwapa moyo wa matumaini naujasiri bila kuwa na ufadhili wa kifedha?

Au mtu huyu anatoka katika maisha gani? Vitali Maembe anatoka katika azingira na maisha wanayoishi watanzania wengi, anajua nini anachoongea, anaongea kitu kinachosemawa na wtanzania wa sasa.

Wenye akili wanaweza kusema nini matokeo ya hii dharau iliyoonyeshwa na Spika, Mawaziri, wabunge na baadhi ya watu waliopata walaka huo ulioambatana na albam ya Muziki ulio andaliwa ili kuwasaidia kuingoza nchi hii nzuri.

Tukiachana na hao Viongozi wetu,

Ndugu watanzania wenzangu,

Nimemaliza awamu ya kwanza ya kugawa Chanjo kwa kufanya onesho Baraza la sanaa tarehe 28 februari 2011. na kufikisha idadi ya watu wasiopungua 20,000 wakiwemo Wanafunzi, walimu, wanasiasa, wazazi, wanahabari, wasanii na watu wa kawaida wamepata Chanjo dhidi ya Rushwa, Uvivu na Ubinafsi.

Pengine inaweza kuwa kazi ngumu sana kulimaliza hili tatizo kwa muda mfupi lakini mimi nawe tukikubali kuwa rushwa ni tatizo, tukianza leo kulitatua tunaweza kuijenga Tanzania bora.

Kwa utafiti nilioufanya kwa kina sisiti kusema kuwa huu ndio wakati pekee ambao tuna weza kuikoa nchi yetu kwa Kalamu na Midomo yetu, tukisubiri kitambo hiki kipite watoto wetu watatakiwa kuiokoa nchi hii kwa gharama kubwa sana, sipendi kulitaja neno damu lakini huko ndiko tunakoelekea. Bado hatupaswi kufikia huko maana kama sisi tukikubali kuumia kidogo leo tutaepusha maumivu makubwa kwa watoto na wajukuu zetu.

Mimi leo nakupa nyimbo zisizopungua 14 kwenye albam ya Chanjo, nakupa nyimbo zisizopungua 32 uzisikilize na ziwe chanjo kwako, napita mtaa hadi mtaa, shule hadi shule, bila ghrama yoyote njoo upate chanjo ili tuliokoe taifa letu.

Naamini kuwa kama nitakubali kumwaga Jasho langu leo, kesho mwanangu hatomwaga damu. Siamini katika pesa, siamini katika mali, bali naamini katika ukweli. Nitaimba kwaajili ya nchi yangu mpaka wasioelewa waelewe. Ungana na mi kama una mapenzi mema na nchi hii. Pata chanjo eneza chanjo… sikiliza muziki wa Vitali Maembe, hudhuria maonesho ya Vitali Maembe leo wakati huitaji kutoa lolote ili upate elimu au burudani.

Mungu ulisha ibariki Tanzania, Mungu ulisha ibariki Afrika, chonde usituondolee Baraka hii.

 
7 Comments

Posted by on March 18, 2011 in Chanjo tour

 

Tags: , , , , , , , , , ,