RSS

Archives

Aside

Mafuriko

Nchi ya demo – ghasia

‘Nchi imetiwa Giza  nasema mimi Mswahili’

Ninaandika kitu kama kitabu lakini wacha niwamegee waswahili wenzangu machache yaliyomo, maana siku za mtanzania zinahesabika na si ajabu ukasikia mswahili hayupo na pengine usisikie lakini ukajua kuwa hayupo maana hutamuona. Katika huo mfano wa kitabu kuna sehemu nimeiita Mafuriko nilikuwa naizungumzia hali ya nchi na urithi wa imani kwa watoto wetu wa leo na wa kesho.

‘Tumepigwa ugenini na nyumbani’ hivyo ndivyo nilivyomsikia jirani yangu Abdallah Punje analalamika akimaanisha tumefungwa mechi zote ya ugenini na ya nyumbani. Nililikamata gita langu nikazivuta siku zijazo nikazilinganisha na hizi zilizopo nikatengeneza maisha ya siku hizo leo. Nikaimba, niliimba weeeh sauti ikakauka, nitaimba tena sauti ikirudi. ‘Tumepigwa ugenini na nyumbani’

Mvua

Mi naapa hii wala sio yetu, hii mvua sio yetu, imetunyeshea  basi tu!

‘Wingu limetanda Magharibi tunanyeshewa sisi Mashariki’ nilicheka sana kwa maana ya kwangu na sio ya msemaji nikizani kuwa msemaji anamaanisha kuwa ‘Wingu limetanda Jioni tunanyeshewa sisi Asubuhi’ kumbe nimenoa, pamoja na kutambua kuwa magharibi ndipo linapotua na Mashariki ndiko lichomozako Jua, na kujiridhisha kuwa anamaanisha wingu limetanda Jioni ‘magharibi’ tumenyeshewa sisi Asubuhi ‘mashariki’ maana ya maneno nimeitambua utata ulikuwa kwenye kujua maana ya maana, maana ya maana bado inasumbua. Labda anamaanisha kuwa Wingu limetanda nchi za Magharibi lakini mvua inatunyeshea sisi huku kwetu, nahisi itakuwa hivyo ndio maana akasema mvua hii si yetu. Tutaharibu mbegu bure tukijifanya wapandaji kwa mvua isiyo yetu.

KUDU

‘Kudu ukudulie umande Masika haikuduliwi’ waswahili wanasema na walisema zamani. Katika utoto wetu tuliwahi kuimba ‘mvua njoo katalina usije’ nikafikiri kuwa maana yake ni mvua njoo Radi usije, na radi tuliyokuwa tunaiogopa sisi ni Ngurumo, mwanga ulikuwa si kitisho kwetu. Miaka michache ya nyuma huko nchi za Asia kumetokea Kimbunga wanakiita Katrina kimezua mafuriko na uharibifu mkubwa wa watu na mali zao, nikashtuka na kujiuliza huyu Katrina ndiye yule Katarina tuliyekuwa tunamuimba asije ije mvua tu? Na kama ndiye huyu mbona wataalamu wanasema kimbunga kama hiki hakijawahi kutokea Duniani miaka mia nyingi zilizopita, inakuwaje leo miaka ya alfu tisa mia themanini mtoto wa kiafrika anaiimba? Hili niwaachie wataalamu wa historia walichimbe mimi wacha niendelee na haya yangu

Kudu ukudulie umande Masika haikuduliwi’  

Huu ni msemo wa Thadhari, mliozoea kuona vimaji kwenye nyasi mkavikudulia hii ni zaidi ya masika.

Umande wa kwenye nyasi waweza ‘ukaukudulia’ ukunyanyua nguo yako ukapita lakini kuna Masika, si mvua ya kitoto, huacha nyasi zimelala au kuchanika chanika. Hupiga mchana kutwa na usiku kucha. Huombwa kwa Sadaka, kafara  na matambiko ikichelewa kufika na masika inapoanza wakulima huwaambia watoto wao wacheze kwenye mvua kufurahia ujio wake, kuonesha kuwa wameikubali na kuiomba isiwakimbie, na watu wanaoikimbia mvua hufukuzwa kijijini maana wanaonesha kuikataa. Natia msemo wangu kidogo  ‘Mkulima hakimbii mvua’

Lakini tusisahau Wakulima wa Mpunga na wa Chumvi hawaivi

Mmoja aomba mvua mwingine aomba jua, usione vitu vinapatana kwenye sufuria ukafikiri huko vitokako kuna amani. Utachekwa.

Sisi watumiaji wa chumvi na mpunga tuna sababu ya kufarakana kwa mambo tunayozani tunayajua na hatuyajui? Tutaishia wapi? Kula wali bila chumvi au kubwia chumvi tupu? Labda nimezungumza lugha ngumu ngoja nizungumze tafsiri ya haya baadhi ya haya, labda nasema kitu kingine ambacho unaweza kuking’amua lakini pia nina maana ya kuwa Migogoro ya tofauti za kiimani si yetu bali inapikwa huko mbali na inatuathiri sisi huku, akili ni nywele sikukatazi wala sikushawishi kujihusisha, amua mwenyewe kwa uwezo wako wa kufikiri na mwisho utakuja kujua kama kujihusisha au kutojihusisha kwako kulikuwa kwa namna gani na kumeisaidia nini asili yako na Nchi yako na ndugu zako. Nanyi viongozi mnatuambia nini juu ya hili? Nyinyi mnajua la kufanya maana kabla hamjajihusisha nyinyi mnahusika sasa kabla hamja litatua msitumie vibaya ndimi zenu maana kauli ya mzee ni dawa.

Kudu ukudulie umande Masika haikuduliwi’  ‘Wingu limetanda Magharibi tunanyeshewa sisi Mashariki’ Hii mvua si yetu mashamba yaandaeni lakini msirogwe kupanda mbegu. Nawaambia mimi Mswahili.

 
1 Comment

Posted by on February 21, 2013 in Uncategorized